Serikali ya Russia imetangaza katika taarifa kwamba ili kuleta uthabiti katika soko la ndani la nishati, imepiga marufuku kwa muda usafirishaji wa petroli na dizeli kwa akthari ya nchi duniani.
Kwa mujibu wa Reuters, Naibu Waziri wa Nishati wa Russia Pavel Sorokin ameeleza katika taarifa kwamba, marufuku hiyo ni ya muda usiojulikana na hatua zaidi zitategemea kutoshelezeka kwa soko la ndani.
Sorokin ameongezea kwa kusema: kizuizi hicho cha muda kitajaza soko la ndani la mafuta na kupunguza bei yake kwa watumiaji.
Kulingana na ripoti hiyo, usafirishaji wa petroli na dizeli kwa nchi nne za Belarus, Kazakhstan, Armenia na Kyrgyzstan haujumuishwi katika marufuku hiyo iliyotangazwa na Moscow.
Katika miezi iliyopita,Russia imekabiliwa na uhaba wa mafuta ya petroli na dizeli, ambayo hatimaye imepelekea kuongezeka kwa bei ya nishati hizo.
Hali hiyo ya ughali wa nishati imekuwa mbaya zaidi katika baadhi ya sekta za kilimo kusini mwa nchi, ambazo ziko katika msimu wa mavuno.
Wadadisi wa mambo wanasema, matengenezo ya viwanda vya kusafisha mafuta na kushuka kwa thamani ya ruble ya Russia ambayo huchochea usafirishaji wa mafuta nje, ni miongoni mwa mambo ambayo yamesababisha mvutano katika soko la ndani la mafuta la Russia…