Utawala uliowekwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwishoni mwa mwezi wa Julai umekaribisha tangazo la Emmanuel Macron la kujiondoa kwa wanajeshi wa Ufaransa waliotumwa nchini humo na kuondoka kwa balozi wa Ufaransa.
“Jumapili hii, tunasherehekea hatua mpya kuelekea uhuru wa Niger,” wamepongeza wanajeshi walio madarakani nchini Niger Jumapili, Septemba 24, katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa.
“Wanajeshi wa Ufaransa pamoja na balozi wa Ufaransa wataondoka katika ardhi ya Niger ifikapo mwisho wa mwaka. Huu ni wakati wa kihistoria ambao unashuhudia dhamira na nia ya raia wa Niger,” taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imesema.
Kwa kumaliza mvutano wa miezi miwili na utawala wa kijeshi wa Niger, Rais Emmanuel Macron hatimaye kutangaza siku ya Jumapili kurejea Paris kwa balozi wa Ufaransa nchini Niger na kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Niger “mwishoni mwa mwaka”.
Kujiondoa huku kwa wanajeshi 1,500 wa Ufaransa walioko Niger, ambayo kabla ya mapinduzi ya Julai 26 ilikuwa mmoja wa washirika wa mwisho wa Paris katika Sahel, kunakuja baada ya wale kutoka Mali na Burkina Faso, ambapo Ufaransa ilishinikizwa na tawala za kijeshi katika nchi zo kuwaondoa.