Serikali ya Somalia na Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wamelaani shambulizi la bomu la kujitoa mhanga lililotekelezwa na magaidi wa al-Shabab Jumamosi mjini Beledweyne, katikati mwa Somalia, na kusababisha vifo vya takriban watu 20, na wengine wengi kujeruhiwa.
Katika taarifa tofauti zilizotolewa na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, na mwakilishi maalum wa mjumbe wa mwenyekiti Tume ya AU ya Somalia na mkuu wa ATMIS Mohammed El-Amine Souef, wameahidi kuongeza juhudi za kuleta utulivu nchini Somalia licha ya kuongezeka kwa mashambulizi kutoka kwa kundi la Al- Shabaab.
Rais Mohamud ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa watu waliouawa, na salamu za pole kwa majeruhi, na kuahidi kuwa serikali ya Somalia na watu wake hawatakata tamaa katika mapambano yao dhidi ya magaidi na ajenda zao mbaya.
Maafisa wa uokozaji wanasema, miili zaidi imepatikana na idadi ya watu waliopoteza maisha, sasa imefikia zaidi ya 20, idadi ambayo hata hivyo huenda ikaongeza kwa mujibu wa maafisa hao.
Shambulio hilo lilitokea baada ya mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye lori hilo kulipuka na kusababisha kuanguka kwa jengo lililokuwa karibu.
Polisi wanasema polisi wanasema wanaendelea na harakati za kutafuta miili zaidi katika shambulio ambalo liliwaacha watu wengine zaidi na majeraha mabaya.