Washington itazingatia hatua zote za siku zijazo kuhusu uwepo wake wa kijeshi nchini Niger, kufuatia tangazo la Ufaransa kwamba itaondoa wanajeshi wake nchini humo mwishoni mwa mwaka, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema Jumatatu.
“Huku tukiipa nafasi diplomasia, tutaendelea pia kuchunguza hatua zote zijazo ambazo zitaweka kipaumbele malengo yetu ya kidiplomasia na usalama,” Lloyd Austin aliuambia mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, ambako anazuru.
Rais Emmanuel Macron alitangaza Jumapili kurejea Paris kwa balozi wa Ufaransa mjini Niamey na kuwaondoa kutoka Niger wanajeshi 1,500 wa Ufaransa walioko nchini humo.
“Tunasitisha ushirikiano wetu wa kijeshi na mamlaka ya ukweli nchini Niger, kwa sababu hawataki tena kupambana na ugaidi,” alisema rais wa Ufaransa.
Marekani ina takriban wanajeshi 1,100 walioko Niger, wakipambana na makundi ya kijihadi yanayofanya kazi katika eneo hilo.
“Hatujafanya mabadiliko yoyote muhimu kwenye nafasi ya vikosi vyetu na tunataka suluhu la kidiplomasia, matokeo ya amani”, alihakikishia Waziri wa Ulinzi wa Marekani, ambaye alikataa kutoa maoni yake kuhusu uamuzi wa Paris.
Pentagon ilikuwa imetangaza mnamo Septemba 7 kwamba ilikuwa inawaweka tena wanajeshi wake “kama tahadhari”, kuwahamisha baadhi ya wanajeshi kutoka kambi ya mji mkuu Niamey hadi kambi ya wanahewa kaskazini zaidi.
Mnamo Septemba 14, Marekani ilitangaza kuwa inarejelea safari za ndege za uchunguzi juu ya Niger, ambayo ilikuwa imekatiza baada ya mapinduzi ya kijeshi mwishoni mwa Julai huku operesheni zake zilizosalia za kijeshi nchini zikibaki zikiwa zimehifadhiwa, msemaji wa Pentagon alisema.