Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu (OHCHR) imetangaza kuwa, mauaji ya halaiki yameongezeka nchini Myanmar.
Ripoti ya Ofisi ya Kamishna Mkuuu wa Haki za Binadamu inasema, jeshi la Myanmar liliongeza ukandamizaji wake kwa mauaji ya watu wengi, mashambulizi ya anga na mizinga katika kipindi cha mwaka uliopita wakati likipambana kuzima upinzani dhidi ya wanaopinga mapinduzi yake.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu (OHCHR) imegundua “msururu wa ghasia za kijeshi” kati ya mwezi Aprili 2022 na Julai 2023, ilisema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu Myanmar.
OHCHR ilitoa mfano wa shambulio la anga kwenye mkutano uliofanyika katika kijiji kwenye ngome ya upinzani mwezi Aprili, na kusema kuwa watu wapatao 150 waliuawa, na shambulio la bomu la Oktoba mwaka jana katika tamasha la waasi lililofanyika kaskazini mwa jimbo la Kachin ambako dazeni ya watu waliuawa.
Kwa mujibu wa taasisii hiyo, mara kwa mara, wanajeshi wamekuwa wakifanya vitendo vya ubakaji na mauaji holela kwa wanaume, wanawake na watoto katika vijiji vinavyoshukiwa kuwahifadhi au kuwaunga mkono wapiganaji wanaopinga mapinduzi.