Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa nyakati tofauti imetoa elimu kwa Wananchi wa Wilaya za Gairo na Mvomero mkoani Morogoro lengo likiwa wananchi watambue pamoja na kufahamu majukumu ya tume hiyo
Akizungumza na wananchi hao kwa nyakati tofauti Naibu katibu wa Maadili na nidhamu Tume ya Utumishi wa Mahakama Alesia Mbuya amesema wananchi wengi wanakumbana na Changamoto pindi wawapo mahakamani kwa kufanyiwa Vitendo visivyo vya kimadili na maafisa wa Mahakama lakini hawajui wapi kwa kuwasilisha malalamiko hayo.
Mbuya amesema Tume ya utumishi imegawanya majukumu yake ambapo kwa ngazi ya Wilaya kunakua na Kamati za maadili ya maafisa wa mahakama ngazi za Wilaya huku Mkuu wa wilaya akiwa ndio mwenyekiti na Katibu tawala akiwa katibu wa tume hiyo .
Anasema pia kuna kamati ya maadili maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa ambapo mkuu wa mkoa ndiye mwenyekiti wa kamati na Katibu tawala ndiye katibu wa kamati hiyo.
Mbuya anasema baadhi ya Vitendo visivyo vya kimaadili ambavyo mwananchi anatakiwa kuwasilisha kwenye kamati kwa njia ya maandishi au mdomo ni pamoja na Matusi ,rushwa au kutolewa lugha ya kuashiria ubaguzi ambayo vinaweza kufanywa na mtendaji wa mahakama aidha, hakimu, karani au mlinzi.
Malalamiko hayo yanatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu Tawala Wilaya (DAS) kwa ngazinya Wilaya na Kwa ngazi ya Mkoa (RAS) ndiye yatapelekwa kisha kupeleka kwa mwenyekiti wa kamati ili taratibu zingine za kujadili ziendelee.
Kwa upande wake Enziel Mtei Naibu Katibu Tume ya Utumishi wa Mahakama Ajira na Uteuzi amesema wananchi wanatakiwa kuwa na imani na kamati hízo kwani zipo kisheria hivyo wanapaswa kufuata taratibu ili waweze kupata haki zao.
Naye mkuu wa wilaya ya Mvomero Judith Nguli amesema atahakikisha kamati yake inatenda haki kwa kila mtu ili isimuone mlalamikaje au mlalamikiwa.
Nao wananchi wameishukuru Tume hiyo ya Utumishi wa Mahakama hiyo kwa kutoa elimu ambayo wanaamini itakua mkombozi katika masuala ya kisheria.