Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishnaa Msaidizi wa Polisi Edith Swebe akiwa amengozana na Mkuu wa Polisi Jamii mkoani humo ACP Mayunga R. Mayunga ametoa elimu ya uvuvi salama kwa Wananchi wa Vijiji vya Mwaburugu, Nyamikoma na Ihale Wilayani Busega katika fukwe za Ziwa Victoria.
Kamanda Swebe ameitaka jamii inayojishughulisha na uvuvi kuzingatia usalama wao kwanza kwa kuchukua tahadhari zote kwa kuzingatia taratibu na kanuni za uvuvi.
Aidha, kamanda Swebe ameendelea kuwakumbusha juu ya wajibu wao na amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu wanajihusisha na uhalifu ndani ya ziwa Victoria na kutoa wito kwa wenye tabia hizo waache mara moja maana Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limejipanga kuzuia uhalifu na wahalifu kwa kufanya doria na misako ya mara kwa mara katika maeneo yote yanayozunguuka Ziwa Victoria na kuhakikisha kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kwenda kinyume na kanuni na taratibu.
Aliongeza kuwa, ni vyema kujiepusha na vitendo vya uvuvi haramu wa kutumia milipuko, nyavu aina ya kokoro ambazo zinasababisha uhalifu wa mazao ya ziwani.
Kamanda Swebe yupo kwenye ziara ya kuhakikisha makundi yote kwenye jamii yanafikiwa na elimu ya Polisi jamii ikiwa ni mkakati wa kuishirikisha jamii katika kutambua viashiria vya uhalifu na wahalifu pamoja na kukemea vitendo vinavyohatarisha ukuwaji wa uchumi.