Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, takribani watu 186,000 wamewasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterania mwaka huu.
Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR mjini New York Ruven Menikdiwela ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba watu 130,000 wamesajiliwa nchini Italia idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita wa 2022.
Menikdiwela ameeleza kuwa, zaidi ya watu 2,500 hawajulikani waliko au wamekufa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 24.
Hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa, zaidi ya watu 2,700 hawajulikani waliko au wamekufa.
Ongezeko la idadi ya wahamiaji tayari limesababisha mivutano ndani ya Umoja wa Ulaya juu ya hatua za kudhibiti wimbi la wahamiaji hao.
Viongozi wa nchi tisa za Mediterania na kusini mwa Ulaya, akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, wanakutana leo nchini Malta kwa mazungumzo yatakayojikita juu ya suala la wahamiaji.
Mkutano huo unafanyika siku moja tu baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR kusema kwamba zaidi ya wahamiaji 2,500 wamepoteza maisha au hawajulikani waliko wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania mwaka huu – idadi hiyo ikiwa juu zaidi ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2022.