Waziri Mkuu wa zamani wa Burundi, Alain-Guillaume Bunyoni, amefikishwa mahakamani siku ya Alkhamisi, akituhumiwa kuhatarisha usalama wa taifa na kumtusi rais.
Alain-Guillaume Bunyoni, ambaye alikuwa Waziri Mkuu tangu mwezi Juni 2020, alifutwa kazi mnamo mwezi Septemba 2022, siku chache baada ya rais Evariste Ndayishimiye kushutumu majaribio ya “mapinduzi ya serikali”. Nafasi yake ilichukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Gervais Ndirakobuca.
Kwa muda mrefu Bwana Bunyoni alikuwa akichukuliwa kuwa ndiye kiongozi nambari mbili wa kweli wa utawala na kiongozi wa watu wenye msimamo mkali kati ya majenerali wanaoshikilia madaraka. Alikamatwa mwezi Aprili mwaka huu katika mji mkuu wa kiuchumi Bujumbura, na tangu wakati huo anazuiliwa katika mji mkuu Gitega. Kesi ilianza mbele ya Mahakama ya Juu, ambayo ilisikizwa gerezani.
“Jenerali Bunyoni alionekana na washtakiwa wenzake sita katika chumba kilichokarabatiwa vizuri katika gereza kuu la Gitega, asubuhi ya Alhamisi kuanzia saa tano mchana hadi saa saba, mbele ya karibu watu hamsini akiwemo mmoja wa binti zake,” chanzo cha mahakama ambacho kimeombwa kutotajwa jina kimeliambia duru za habari.