Mahakama moja nchini Ushelisheli imemshtaki kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na watu wengine saba kwa tuhuma za uchawi.
Patrick Herminie anapanga kugombea katika uchaguzi wa urais wa 2025 chini ya bendera ya United Seychelles Party (USP), chama kikuu cha upinzani nchini humo.
Hata hivyo, amekanusha mashtaka hayo.
Aliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka ni juhudi za kisiasa za kuchafua taswira yake na ya chama chake.
Polisi wanasema kisa hicho kinahusiana na kupatikana kwa miili miwili iliyokuwa imetolewa kwenye makaburi katika kisiwa cha Mahe.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini, Bw Herminie na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupatikana na vitu vilivyokusudiwa kutumiwa katika uchawi na kula njama ya kufanya uchawi.
Polisi wanasema walimpata Bw Herminie akiwa na stakabadhi zinazoshukiwa kuibwa kutoka maeneo yaliyoharibiwa, yakiwemo makanisa ya Kikatoliki.
Pia wanadai kuwa jina la Bw Herminie lilionekana kwenye mawasiliano ya Whatsapp kati ya raia wa Ushelisheli na Mtanzania ambaye alikamatwa Septemba akiwa na vitu vinavyohusiana na uchawi.