Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam wamesaini mikataba ya Shilingi Bilioni 9.34 kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali ikiwemo barabara ya mtaa wa Msikitini katika jimbo la Ilala.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo baina ya Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Haruin Rashid Senkuku na Wakandarasi hao huku Wakuu wa Idara mbalimbali wakishuhudia ambapo amewataka kufanyakazi ya viwango na kikamilifu ili kuepuka visingizio.
“Tunajua wote kuwa kuna matarajio ya uwepo wa mvua za El nino kama ilivyotangazwa na mamlaka husika; Hivyo mikataba tumesaini leo ni bora kazi ianze mapema maana kila kitu kipo zikiwemo na fedha ; isitokee sababu baadaye kwamba mmeshindwa kufanyakazi kwa wakati kwa sababu ya mvua,”.
Mbali na barabara ya Msikitini katika mkataba huo uliowahusisha Wakandarasi Tisa, pia barabara nyingine zitakazojengwa ni Makabe – Msakuzi, Kibamba shule Magoe mpiji; Chanika -Mbande na Barabara za mitaa ya Kipata na Livingstone iliyopo kariakoo katikati ya jijini la Dar es salaam.