Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema katika ripoti yake mpya kwamba wahamiaji haramu 271 waliokolewa katika pwani ya Libya wiki iliyopita.
Katika taarifa yake hiyo, IOM imesema kuwa, wahamiaji hao, ambao wamo pia wanawake 25 na watoto 23, waliokolewa na kurejeshwa Libya kati ya Septemba 24 na 30 na kuongeza kwamba, maiti wa watu wanne wameopolewa majini kwenye kipindi cha tarehe hizo mbili.
Taarifa hiyo aidha imesema: Hadi sasa kwa mwaka huu, jumla ya wahamiaji haramu 11,736 wameshaokolewa na kurejeshwa Libya, waliokufa ni 925 na 1,168 wametoweka na harajulikani walipo hadi hivi sasa.
Matukio hayo yametokea kwenye njia ya katikati mwa bahari ya Mediterania kwenye pwani ya Libya.
Mwaka jana yaani 2022 pia, wahamiaji haramu 24,684 waliokolewa na kurudishwa Libya, huku 529 wakifa maji na 848 walipotea baharini na mpaka hivi sasa hawajapatikana.