Shirika lisilo la kiserikali la Compassion Tanzania limezindua mpango wa miaka mitano utakao fikia vijana na watoto zaidi ya milioni 1.7 (milioni moja na laki saba) walio kwenye mazingira hatarishi kwenye eneo la ulinzi wa mtoto, afya, lishe, maji, mazingira na kuinua uchumi wa kaya.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo uliofahamika kama our neighbor promise 2027 strategy mkurugenzi wa shirika hilo Mary Lema amesema watawafikia watoto hao kutoka mikoa 21 ya Tanzania kupitia makanisa zaidi ya 500 wanayofanyanayo kazi kwa karibu.
Kwa upande wake Kamishna wa ustawi wa jamii Dkt. Nandera Mhando ametoa rai kwa watu wote wenye nia ya kuwasaidia watoto ambao wamefanyiwa vitendo vya ukatili kuto kuwaonyesha sura zao kwani jambo hilo litawaathiri maisha yao yote.
Naye kaimu M/Kiti wa bodi ya shirika hilo Dkt.Elieshi Kisinza amesisitiza wadau kuungana pamoja katika kutetea haki za watoto na si kuacha kazi hiyo mikononi mwa shirika pekee.
Shirika la Compassion Tanzania ni shirika la kikristo lililoanzishwa mwaka 1999 lipo katika mikoa 21 na zaidi ya halmashauri 80 ndani ya makanisa 550 na hadi hivi sasa limewafikia watoto 115,000 (Laki moja na elfu 15).