Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amemkabidhi kazi ya ujenzi mkandarasi kampuni ya China Henan Internation Cooperation Group Ltd (CHICO) atakayejenga barabara ya njia nne kutoka Igawa, Mbeya Songwe hadi Tunduma, yenye urefu wa kilometa 218 kwa kiwango cha lami.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mbalizi Mkoani Mbeya, Waziri Bashungwa amesema Serikali itatumia zaidi ya Sh1.1 trilioni kukamilisha ujenzi barabara hiyo itakayotoka Igawa Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya mpaka Mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Zambia.
Dhamira ya Rais Samia Suluhu ni kuijenga barabara hii kwa viwango vya Ulaya ,:- ameongeza kuwa Barabara hii itachochea kasi ya maendeleo kwa nchi za SADC, lakini pia itapunguza msongamano wa magari katikati ya mji kwani mbali na ujenzi wa barabara hii pia, fedha zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Malori itayoanzia Uyole hadi Songwe.
Aidha Waziri Bashungwa amesema alipoapishwa alielekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kushughulikia kwa karibu ujenzi wa barabara hiyo ikiwezekana ahamie mkoani hapo kwani amechoka kusikia kero ya msongamano kwa wana Mbeya.
“Mkandarasi najua umeshasalimia njoo, njoo nikutambuluishe kwa wanambalizi na wana Mbeya watakapokuwa wanaona mitambo ya magreda inatengeneza barabra wajue pochi la mama limetema, amewapatia fedha chiko ili barabara ianze kujengwa”
Pamoja na hayo Waziri Bashungwa ametoa wito kwa wananchi wa Mbeya na maeneo ambayo barabara hiyo itapita kumpa ushirikiano wa kotosha mkandarasi CHICO ili aweze kufanya kazi yake haraka na kwa weledi mkubwa.
Amesema amejiridhisha na weledi wa mkandarasi huyo kwa kuangalia vifaa vyake pamoja na wataalaamu, watakaoratibu kwa karibu ujenzi wa barabara hiyo hivyo hana wasiwasi kabisa kwamba barabara hiyo itajengwa kwa ubora.