Karibia raia 400 nchini Misri wamekamatwa kwa kuhusishwa na maandamano yaliyotokea baada ya rais Abdel Fattah al-Sisi, kutangaza kuwania urais kwa awamu ya tatu, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.
Hatua hiyo ya rais Sisi, siku ya Jumanne ilionekana kuzua ghadhabu kutoka kwa raia kwenye taifa hilo, baadhi ya vídeo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikonyesha maandamano yaliofanyika katika mji wa Marsa Matrouh, kaskazini mashariki mwa taifa hilo.
Baadhi ya waandamanaji katika vídeo hiyo wanasikika wakiimba nyimbo za kumtaka rais Sisi kuondoka pamoja na utawala wake.
Video nyengine zilionyesha makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.
Kiongozi huyo wa zamani wa jeshi amekuwa madarakani tangu kuangushwa kwa utawala wa Mohammed Morsi, mwaka wa 2013 kufuatia maandamano makubwa dhidi ya uongozi wake.