Programu ya mitandao ya kijamii TikTok inasitisha huduma yake ya ununuzi mtandaoni nchini Indonesia ili kutii sheria mpya katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Kusini Mashariki mwa Asia.
Hatua hiyo itaanza kutekelezwa saa 17:00 saa za Jakarta (10:00 GMT).
Serikali ya nchi hiyo inasema kanuni hizo zinalenga kusaidia kuwalinda wauzaji bidhaa wa ndani na wa mtandaoni.
Indonesia ilikuwa nchi ya kwanza kufanya majaribio ya huduma ya e-commerce mnamo 2021 na TikTok ikawa moja ya soko kubwa la ununuzi.
Wiki iliyopita, Indonesia ilitangaza kanuni ambazo zingelazimisha TikTok kugawa kipengele chake cha ununuzi kutoka kwa huduma maarufu ya kushirikisha video nchini humo.
Akitangaza hatua hizo, waziri wa biashara wa Indonesia Zulkifli Hasan alisema: “Sasa, biashara ya mtandaoni haiwezi kuwa mitandao ya kijamii. Imetenganishwa.”
Pia aliambia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwa walikuwa na wiki moja ya kufuata sheria hizo mpya la sivyo watapoteza leseni yao ya kufanya kazi nchini.
Tangazo hilo linawadia baada ya Rais wa Indonesia Joko Widodo kusema mwezi uliopita: “Tunahitaji kuwa makini na biashara ya mtandaoni. Inaweza kuwa nzuri sana ikiwa kuna kanuni lakini inaweza kuwa mbaya ikiwa hakuna kanuni zozote.”
“Kipaumbele chetu ni kubaki kuzingatia sheria na kanuni za eneo,” TikTok ilisema katika taarifa Jumanne .
“Kwa hivyo, hatutawezesha tena shughuli za biashara ya mtandaoni katika Duka la TikTok Indonesia,” iliongeza.