Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa(Mb) amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa-Kilolo (km 33.61) kwa kiwango cha lami utakapokamilika utaleta mageuzi chanya na kuchochea fursa nyingi katika Sekta ya Kilimo, Utali, Biashara na Uwekezaji.
Bashungwa ameeleza Oktoba 5, 2023 wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS), na Meneja Mkazi kutoka kampuni ya Hunan Construction Engineering Group na kumtambulisha mkandarasi huyo kwa wananchi.
“Hakika historia inaenda kuandikwa kwani barabara ya Iringa – Kilolo imekuwa ni kilio cha muda mrefu, kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Iringa na hasa wale ambao walikuwa wawakilishi wenu kupitia Jimbo hili kwa nyakati tofauti tofauti pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wameisemea sana barabara hii”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutawezesha wananchi kiuchumi, na kuwaondolea adha ya muda mrefu ya usafiri.
Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifahamu adha ya wana Iringa na mikoa jirani katika eneo la Kitonga na amemuagiza kufika na timu ya Watalaam kutoka TANROADS na kufanya tathimini ya ujenzi wa barabara ya mbadala ya muda mfupi wakati Serikali ikiendelea kutafuta dawa ya kudumu katika eneo hilo lenye mlima mkali.