Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA inaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vinne Mkoani Mwanza na sasa ujenzi wa vivuko hivyo umefikia 67%.
Ujenzi huo wa vivuko vipya unafanywa na kampuni ya Mtanzania Songoro Marine iliyoko Jijini Mwanza, huku wakisimamiwa na wataalamu kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania TEMESA.
Vivuko hivyo vinne vinavyojengwa ni pamoja na kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala wilayani Magu, kivuko kingine ni kati ya Bwiro na Bukondo walayani Ukerewe, kivuko kati ya Kisorya na Rugezi wilayani Ukerewe pamoja na kivuko kati ya Nyakaliro na Kome wilayani Sengerema vyote vikiwa Mkoani Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kukagua vivuko hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri TEMESA Mhandisi. Deogratias Nyanda amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 61, kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vipya pamoja na ukarabati wa vivuko vinavyoendelea kutoa huduma kote nchini.