Rais wa Kenya William Ruto ataomba China mkopo wa dola bilioni 1 ili kukamilisha miradi ya barabara iliyokwama atakaposafiri hadi Beijing baadaye mwezi huu, naibu wake Rigathi Gachahua alisema Ijumaa.
Akiongea kwenye redio ya humu nchini Inooro FM, Gachahua alisema kuwa Ruto pia ataomba muda mrefu zaidi wa kulipa pesa ambazo tayari zinadaiwa.
Kwa sasa Kenya inadaiwa zaidi ya dola bilioni 8 za mikopo ya China.
Mpango huo wa Ruto ni mabadiliko makubwa katika msimamo wake, baada ya muungano wake hapo awali kukashifu mtangulizi wake Uhuru Kenyatta wa kukopa kutoka Uchina.
Awali Kenyatta alitumia mikopo ya Uchina kufadhili miradi ya miundombinu, kama vile barabara kuu ya Nairobi, lakini mingi ya miradi hii imekwama kutokana na wanakandarasi kuiacha kwa sababu ya bili ambazo hazijalipwa.
“Tukipata dola bilioni 1 tunaweza kuwapa watu hawa [wakandarasi] pesa wanazodaiwa ili waweze kurejea kwa hivyo hata tunapolipa deni, barabara zimekamilika,” Gachahua alisema.
Naibu huyo alisema Ruto atawauliza maafisa wa Uchina ikiwa Kenya inaweza kupewa muda zaidi wa kulipa madeni hayo.