Watu saba wamefariki dunia na wengine 22 wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la Kiwawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, ikihusisha basi la kampuni ya Saibaba linalofanya safari zake Nachingwea kwenda Dar es salaam na basi dogo la kampuni ya Baharia linalofanya safari zake Dar es salaam kwenda Tandahimba.
Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Pili Mande amesema chanzo cha ajali hiyo ni basi la kampuni ya Saibaba kutaka kulipita gari kubwa la mizigo ambalo lilikuwa mbele yake na ndipo likakutana na basi hilo dogo la kampuni ya Baharia likitokea Dar es Salaam na kugongana uso kwa uso.
Waliofariki Dunia ni Lucas John (59) Dereva wa basi la Saibaba (Mkazi wa Arusha) ambaye amefariki papohapo na Omari Alli Abdalah (49) ambaye ni Dereva wa gari ndogo ya Baharia “Miili ya Watu wengine watano bado haijatambuliwa majina yao mpaka sasa”
“Majeruhi watatu ambao hali zao ni mbaya majina yao hayajafahamika ambapo kati yao Wanawake ni wawili na Mtoto mdogo wa kiume wote wamelazwa katika Hospitali ya Kinyonga Wilaya ya Kilwa”