NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya UChukuzi DKT Ally Possi ameutaka uongozi wa Kampuni ya Huduma za MELI(MSCL) kufikiria kumiliki vyombo vya Usafiri Baharini.
Dkt Possi amezungumza hayo katika kikao kazi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kuongea na Uongozi , Mkandarasi anayejenga Meli ya MV Mwanza Gas Entec ya Korea Kusini na kupokea Maelezo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL), kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Gold Crest Hotel Jijini Mwanza Leo tarehe 07 Oktoba, 2023.
Dkt Possi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufanya maboresho makubwa kwenye Sekta ya Uchukuzi ikiwemo uwekezaji kwenye Kampuni ya MSCL ili iweze kusafirisha abiria na mizigo zaidi Sasa Kampuni ifikirie kumiliki vyombo Baharini.
“Ukiachilia mbali ujenzi wa Meli mpya ya MV Mwanza,ukarabati MV Umoja Kwa Ziwa Victoria, Mv Liemba na MT Sangara Ziwa Tanganyika, tunakwenda kusaini Mikataba Mitatu Kigoma ya ujenzi wa Kiwanda Cha kutengeneza Meli, ujenzi Meli mpya mbili za Tani 3,500 na 3,000 haya ni mapinduzi makubwa Kwa Usafiri wa njia ya maji kwenye maziwa yetu Sasa tufikirie kwenda Baharini” amesisitiza Dkt Possi
Dkt Possi amesema Kwa upande wa Baharini Kuna mizigo mingi ambayo tukitumia fursa vizuri tutaihudumia kutoka na kwenda maeneo ya Comoro, Shelisheli na hata Dubai na kuitaka Kampuni hususani kitengo Cha masoko kuboresha mbinu za kibiashara.
Akizungumzia mikakati ya Kampuni na miradi inayoendelea , Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Eric Hamissi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita sambamba na Wizara ya Uchukuzi Kwa kuendelea kutoa fedha Kwa maboresho mbalimbali ya rasilimali za Kampuni ikiwemo ukarabati wa Meli ya Mv Umoja uliotumia zaidi ya shilingi Bil 18 ambao umekamilika na Meli imerudi kuwa mpya kabisa na imeshaanza kufanya kazi.
Bw. Eric ameongeza kuwa Kampuni hiyo inatekeleza mradi wa ujenzi wa Meli Mpya ya Mv Mwanza ambao ujenzi wake umefikia asilimia 90 na Ukarabati wa MT Sangara uliofikia asilimia 92 yote ikitarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka ujao na Mikataba ya miradi zaidi itasainiwa wiki ijayo.
“Katika maboresho yanayoendelea chini ya Serikali ya Awamu ya Sita wiki ijayo Tarehe 11 Oktoba, 2023 tutasaini Mikataba Mitatu Kigoma ya ujenzi wa Kiwanda Cha kutengeneza Meli na Meli mpya mbili za Tani 3,500 na 3,000 kama Kampuni tunashukuru sana Serikali na natumia fursa hii kuwaalika wananchi wa Kigoma na mikoa ya jirani kuhudhuria hafla hii ili kuunga mkono jitihada za Serikali” amesisitiza Eric
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurigenzib MSCL Meja Jenerali Mst. John Mbungo , amuahidi Naibu Katibu Mkuu kuwa watashikiana na viongozi wa Kampuni na Kwa msaada wa Wizara inapobidi kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye Kampuni unaleta tija Kwa wananchi na Taifa ili thamani ya fedha ionekane.