Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ametoa wito wa kusitishwa mzozo kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, ambao hadi sasa umesababisha vifo vya mamia ya watu kutoka pande zote mbili.
Mkuu huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amezitaka pande zote mbili kurejea kwenye meza ya mazungumzo bila masharti hatua ambayo itatekeleza kanuni ya mataifa mawili ya kuishi bega kwa bega.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, na hasa mataifa makubwa yenye nguvu duniani, kubeba jukumu la kuweka amani na kulinda haki za watu wa Israel na Wapalestina.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka Israel kuheshimu sheria za kimataifa, wakati ikifanya operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Guterres amesema amesikitishwa na tangazo la Israel kuwa ingeweka mzingiro kamili dhidi ya ukanda huo, ikizuia kikamilifu kuingizwa kwa chakula, maji na nishati ya umeme.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya umefuta kauli yake ya awali kuwa unasitisha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina.
Aidha, Waziri Mkuu wa utawalka haramu wa Israel Benjamin Netanyahu amewataka wapinzani ndanii ya utawala huo kuridhia kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa bila masharti yoyote, wakati utawala huo ukiendelea na operesheni za kulipa kisasi dhidi ya Hamas.