Uingereza imekaribisha kuachiliwa kwa wanaume wanne wa Uingereza kutoka kizuizini nchini Afghanistan na kuomba msamaha kwa niaba ya familia zao kwa “ukiukaji wowote wa sheria za nchi”.
“Tunakaribisha na kuthamini kuachiliwa na utawala wa sasa wa Afghanistan kwa raia wanne wa Uingereza waliokuwa wakizuiliwa kwa madai ya kuvunja sheria za Afghanistan,” msemaji wa Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) alisema Jumanne.
“Kwa niaba ya familia za raia wa Uingereza, tunaomba radhi kwa utawala wa sasa wa Afghanistan kwa ukiukaji wowote wa sheria za nchi,” aliongeza msemaji huyo.
FCDO haikubainisha ni nini watu hao walikuwa wameshutumiwa, lakini ilisema raia wote wa Uingereza walitakiwa kufuata “sheria ya Uingereza ya kukabiliana na ugaidi wanapokuwa nje ya nchi na kutii sheria zote za nchi wanakoenda”.
Kundi la Taliban limekuwa likifanya kazi na kudhibiti polisi, idara za ujasusi na magereza nchini Afghanistan tangu walipochukua udhibiti wa nchi hiyo kufuatia kujiondoa kwa Merika na vikosi vingine vya kigeni mnamo 2021.
Nchi nyingi zimewashauri raia wao kuepuka kusafiri kwenda Afghanistan tangu Taliban kuchukua mamlaka.
Ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa ilirekodi zaidi ya matukio 1,600 ya ukiukaji wa haki dhidi ya watu wanaozuiliwa na mamlaka ya Taliban, ikiwa ni pamoja na vitendo vya utesaji na unyanyasaji wa polisi na maafisa wa kijasusi.