Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mwanamke wa kwanza kutunikiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa watoto hususan wa kike wanaoishi katika mazingira magumu nchini.
Akiipokea Shahada hiyo, am ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini, Rais Samia amesema anakishukuru Chuo hicho kwa heshima hiyo ambayo ni kubwa na kwamba anaitoa kwa watoto wa kike wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu na pembezoni mwa nchi ambapo amewaka kutokukata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.
Ameeleza kuwa ameitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa.
Pia amesema anawashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Tanzania kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.
” Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani na baba mwalimu. Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa” amesema Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Santishree Dhulipudi Pandit amesema Chuo hicho kimetunuku Mhe. Rais Samia Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar ameielezea Shahada hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India.