Ufaransa imeanza zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake nchini Niger, baada ya kutimuliwa na baraza la kijeshi linalotawala nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Msemaji wa Kamanda Mkuu wa jeshi la Ufaransa akisema kuwa, “Wanajeshi wetu ambao ni sehemu ya kikosi cha askari 1,400 wameanza kuondoka Niger leo Jumanne, huku wakisindikizwa na vikosi vya Niger.”
Jeshi la Ufaransa limethibitisha habari hiyo ya kuanza kuwaondoa askari wake nchini Niger, siku moja baada ya wakuu wa jeshi wa nchi hiyo Kiafrika kutangaza habari hiyo ya kuanza kuondoka nchini humo wanajeshi wa Ufaransa.
Jana Jumatatu, baraza la kijeshi linalotawala Niger lilitangaza kuwa, limefikia makubaliano na Paris kwa ajili ya kuwaondoa wanajeshi hao wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika.
Habari zaidi zinasema kuwa, wanajeshi hao wa Ufaransa waliofukuzwa kwa madhila nchini Niger wataelekea Chad.
Zoezi la kuondoka wanajeshi wa Ufaransa nchini Niger limepangwa kumalizika mwezi Disemba mwaka huu, wakati askari wa mwisho watakapoondoka katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.