Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, inakabiliwa na pengo kubwa la fedha zinazohitajika kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu nchini Ethiopia.
Katika ripoti ya hivi karibuni kuhusu hali ya nchini Ethiopia iliyotolewa jumatatu jioni, Ofisi hiyo imesema ni asilimia karibu 28.9 ya dola za kimarekani bilioni 3.99 zinazohitajika kushughulikia mahitaji ya kibinadamu nchini Ethiopia ndio zimepatikana.
Ofisi hiyo pia imetoa wito kwa wenzi wa kibinadamu kumalizia pengo la dola za kimarekani bilioni 2.84 zilizobaki ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu nchini Ethiopia kwa mwaka huu wa 2023.
Ripoti hiyo pia imesema fedha hizo ni muhimu katika kuwasaidia watu zaidi ya milioni 20 walioathirika na vurugu, mapigano na majanga ya asili nchini Ethiopia, wakiwemo watu milioni 13 wanaokabiliwa na ukame mkali katika maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo.