Takriban raia saba wameuawa na kukatwa viungo vyao siku ya Jumanne karibu na Rumangabo, takriban kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na shirika la habari la AFP likinukuu chifu wa eneo hilo na mashahidi.
Wakati mapigano yakiongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya jeshi la Congo na wanamgambo wa ndani kwa upande mmoja na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kwa upande mwingine kulingaana serikali ya DRC, watu saba wamepatikana wameuawa kwa kuchinjwa na kukatwa viungo vyao siku ya Jumanne asubuhi kwenye barabara ya kitaifa namba 2, katika eneo la Rutshuru.
Eneo hili lilirejeshwa rasmi na kundi la waasi wa M23 mwanzoni mwa mwaka kwa wanajeshi wa Kenya waliotumwa kama sehemu ya jeshi la Afrika Mashariki, linalopaswa kutoa ulinzi katika eneo lisilo kuwa na wanajeshi au wapiganaji kati ya pande hasimu. Waasi wa M23 walidumisha uwepo na udhibiti wa usafirishaji haramu wa watu na bidhaa kwenye sehemu za barabara ya kitaifa (RN 2) na katika vijiji vya karibu.
Usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, watu “waliovalia sare za kijeshi na wengine waliovaa kiraia” waliwateka nyara watu saba kutoka kwa nyumba zao, akiwemo “chifu wa eneo la Bugoma (karibu kilomita 1 kutoka Rumangabo) na naibu wake”, Patrick Ntamugabumwe, chifu wa eneo la Rumangabo, ameliambia shirika la habari la AFP.