Papa Francis, katika matamshi yake tangu kuanza kwa mzozo huko Gaza, siku ya Jumatano alitoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wote waliochukuliwa na wanamgambo wa Hamas na kusema Israel ina haki ya kujilinda.
Akizungumza kwa sauti kuu mwishoni mwa hadhara yake ya kila wiki kwa maelfu ya watu katika uwanja wa St. Peter, pia alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza.
“Ninaendelea kufuatilia, kwa uchungu na wasiwasi, kile kinachotokea Israel na Palestina. Watu wengi sana waliuawa, na wengine kujeruhiwa. Nawaombea wale familia walioona siku ya sikukuu ikigeuka kuwa siku ya maombolezo, na ninaomba kwamba mateka waachiliwe mara moja,” alisema.
“Ni haki ya wale wanaoshambuliwa kujilinda, lakini nina wasiwasi mkubwa na mzingiro mzima wa Wapalestina wanaoishi Gaza, ambako pia kumekuwa na wahasiriwa wengi wasio na hatia,” alisema.