Mmoja wa wakurugenzi wa Airplanes Africa Limited Dar es Salaam. Ndege ya kwanza kutengenezwa Tanzania imetambulishwa rasmi na kampuni ya Airplanes Africa Limited (AAL) ya mkoani Morogoro.
Ndege hiyo ilitambulishwa rasmi katika maonyesho ya kimataifa ya wazalishaji wa bidhaa za Viwandani Tanzania yajulikanayo kwa jina la Tanzania International Manufacturers Expo 2023 (TIMEXPO) yaliyomalizika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Bw David Grolig alisema kuwa uamuzi wa kuzalisha ndege hiyo umetokana na mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.
Bw Grolig alisema kuwa ndege hiyo aina ya Skyleader 600 ina uwezo wa kubeba abiria wawili (akiwemo rubani) na inakidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaosafiri umbali mrefu.
Alisema kuwa walifanya utafiti wa kina ili kuelewa mahitaji ya wafabiashara ambao mara nyingi hufanya safari za masafa marefu na kutumia muda mwingi njiani.
Alifafanua kuwa kutokana na utafiti huo, waliamua kutengeneza ndege itakayowawezesha wafanyabiashara kusafiri kwa urahisi zaidi na kuhudhuria mikutano mbalimbali nje ya mkoa kabla ya kurejea na kuendelea na shughuli nyingine.
“Tunajivunia kutengeneza ndege ya aina hii ambayo ni muhimu kwa wafanya kibiashara na watu binafsi. Huu ni mwanzo na mwakani tutatengeneza ndege nyingine aina ya Skyleader 500 ambayo ni muhimu kwa matumizi ya kilimo na shughuli zingine.
Ndege zote hizi ni matunda ya ubunifu wa wataalamu wetu wazawa na wa kigeni. Watalaamu wazawa wamepata mafunzo Jamhuri ya Czech na mipango ya kuendelea kutoa mafunzo inaendelea ili kuwa na wataalamu wengi zaidi,” alisema Bw Grolig.
Alisema kuwa umiliki wa ndege hiyo ni rahisi zaidi na wamefanya hivyo ili kuendeleza gurudumu la uchumi kwa Watanzania na wateja wao wan je ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo, Bw. Igor Stratil, alisisitiza kuwa ndege hiyo Na.1 ni matokeo ya utaalamu wa pamoja ya timu ya Tanzania na Czech.
Bw Stratil alisema pia wamefurahi kushiriki katika maonyesho ya TIMEXPO na kuwa washindi wa jumla.
Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, na kushirikisha ambapo jumla ya washiriki 138 washiriki na wageni zaid ya 1,000 walikuwa wanatembelea kila siku.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw Albert Chalamila, ambaye alifunga maonyesho hayo na kuwapongeza waandaaji na kampuni ya AAL kwa maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.
Bw Chalamila alisema kuwa ubunifu wa kutengeneza ndege ni kichochea maendeleo ya teknolojia na nyenzo pekee ya kuvutia wawekezaji wengine na kuchangia ustawi wa jamii.