Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amesema Tasnia ya Habari ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mila na utamaduni wa wananchi wa Afrika.
Naibu Waziri Kundo ameyasema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano naTeknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) katika Mkutano wa Mashirika ya Umma ya Utangazaji Kusini mwa Afrika (SABA) unaofanyika Oktoba 10, 2023 katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
“Tasnia ya Habari ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mila na utamaduni wa wananchi wa Afrika. Jitihada za makusudi lazima zifanyike kupitia vyombo vyetu vya Utangazaji vya Umma vyenye jukumu la kuyatekeleza hayo. Niwaombe washiriki wote kuhakikisha kuwa maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari vya umma yazingatie mtizamo wa kuijengea jamii uwezo wa kujitambua na kujivunia uafrika wao.” Amesema Mhandisi Kundo.
Pia mhandisi Kundo amesema kuwa jitihada za makusudi lazima zifanyike kupitia vyombo vyetu vya Utangazaji vya Umma vyenye jukumu la kuyatekeleza hayo pamoja na kuwaomba washiriki wote kuhakikisha kuwa maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari vya umma yazingatie mtizamo wa kuijengea jamii uwezo wa kujitambua na kujivunia uafrika wao.
Sambamba na hayo Mhandisi kundo amelipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuandaa mkutano huo unaokutanisha wadau mbalimbali barani Afrika na kujadili masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
“Tukio hili la leo ni kati ya matukio makubwa yanayohusu ukuaji wa teknolojia ya habari nchini ambayo yametekelezwa na Wizara kushirikiana na taasisi zake.
Tunapokutana katika tukio hili muhimu nitumie fursa hii kumpongeza sana Dkt. Ayub Rioba Chacha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika letu la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa kufanikisha Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu mkubwa katika visiwa vyetu vya Zanzibar.”
Amesema Mhandisi Kundo