Rais Joe Biden alisema Jumanne kuwa “ wako pamoja na Israeli,” wakati Washington ikijaribu kupunguza mivutano Mashariki ya Kati baada ya shambulizi la kushangaza la kigaidi lililofanywa na wanamgambo Hamas.
Pia aliahidi Washington itaendeleza msaada kwa Israeli kujibu mashambulizi dhidi ya kile alichokiita “ukatili” ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, ikiwemo siyo chini ya Wamarekani 14.
“Katika wakati huu, lazima tuwe wazi kabisa: Tunasimama na Israeli,” alisema. “Tutahakikisha wanacho kila wanachohitaji kuweza kuwahudumia raia wao, kujilinda na kujibu shambulizi hili. Hakuna uhalali kwa ugaidi. Na hakuna kisingizio.”
Kwaupande mwingine Joe Biden amesema Israel ina haki na wajibu wa kujibu mashambulizi ya Hamas mwishoni mwa juma, ambayo aliyaita “kitendo cha uovu mtupu”.
Katika matamshi ya nguvu, alisema Marekani “itasimama na Israel” na kutoa msaada wowote inaohitaji.
Bw Biden alisema Wamarekani wasiopungua 14 wameuawa katika mashambulizi hayo na raia wengine wa Marekani wamechukuliwa mateka.
Katika muhtasari wa baadaye siku ya Jumanne, msemaji wa usalama wa taifa alisema angalau Wamarekani 20 hawakupatikana.
Haijabainika ni wangapi kati ya hao wamechukuliwa mateka na Hamas, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan alisema.
Wanamgambo wa kundi hilo ambalo limeteuliwa kuwa shirika la kigaidi na Marekani, walivunja uzio wa mpaka katika Ukanda wa Gaza katika maeneo kadhaa siku ya Jumamosi na kuanzisha mashambulizi makali zaidi ya mpakani ambayo Israel imewahi kukabiliana nayo katika kizazi.
Takriban watu 1,200 wameuawa nchini Israel tangu Jumamosi. Zaidi ya watu 950 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel ya kulipiza kisasi huko Gaza.