Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maagizo matatu kwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na taasisi zilizoko chini yake, hususan, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TRFA) yakilenga kuweka mazingira mazuri kwa wakulima nchini kuzalisha zaidi, wanapojiandaa kuanza msimu mwingine wa kilimo, mwaka huu.
Maagizo hayo ya CCM yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Komredi Daniel Godfrey Chongolo, ni pamoja na Wizara ya Kilimo kuweka na kutangaza utaratibu wa kulipa malipo ya wakulima wa mahindi, hususan wa mikoa ya Kusini, ukiwemo Mkoa wa Rukwa, ambao mazao yao yalinunuliwa na NFRA na hawajamaliza kulipwa.
Agizo jingine ni kuitaka Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kutoa fedha za kununua mahindi ya wakulima ambayo bado yako kwenye maghala huku msimu mwingine wa kilimo ukikaribia kuanza, hali inayoweza kuathiri uzalishaji wao.
Ndugu Chongolo pia ameagiza Wizara ya Kilimo, kupitia TRFA kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya ruzuku mapema kabla ya msimu kuanza na waipate katika maeneo ya karibu, tofauti na msimu uliopita ambapo kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuwa mbolea hiyo ilichelewa kufika na walilazimika kuifuata umbali mrefu kuipata.
“Kuna suala la malipo ya mahindi…tunaiagiza Wizara ya Kilimo kuwalipa wakulima wa mahindi yaliyonunuliwa na NFRA haraka ili waweze kujiandaa na msimu wa kilimo unaokuja. Lakini pia tunawaagiza Wizara ya Kilimo walete fedha ili NFRA wanunue mahindi ambayo bado yako kwa wakulima.
“Mmemsikia mara kadhaa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza suala la kuhifadhi chakula. Kwa mujibu wa wataalam wetu wa utabiri wa hali ya hewa, kuna dalili za kuwepo kwa El Nino kwenye msimu huu wa mvua, ambayo inaweza kuathiri uzalishaji. Hivyo Serikali lazima iweke mpango wa kununua chakula cha kutosha ili kuwa na uhakika wa chakula,” amesema Chongolo na kuongeza;
“Agizo jingine ni kuhusu mbolea…tunawaagiza wasogeze mbolea karibu ili ipatikane kwa karibu kwa wananchi. Huko nyuma, sehemu kubwa ilishia kupatikana makao makuu ya wilaya. Tunawataka Wizara ya Kilimo wafanyie kazi haya.”
Ndugu Chongolo ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Oktoba 11, 2023, alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mjini, mkoani Rukwa, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku 4 katika mkoa huo.
Maagizo hayo ya Katibu Mkuu Chongolo, yamekuja siku chache baada ya Kiongozi huyo kukutana na malalamiko ya wakulima wa mahindi mara tu alipoanza ziara yake Mkoa wa Rukwa, wilayani Nkasi, Oktoba 8, mwaka huu, akiwa ametokea katika Mkoa wa Katavi, akiendelea na ziara zake za kukataa miradi ya maendeleo, ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, kuhamasisha uhai wa CCM katika ngazi ya mashina na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Mbali na maagizo hayo, Katibu Mkuu Chongolo pia alizungumzia umuhimu wa viongozi na watendaji wa Chama na Serikali katika ngazi mbalimbali, kushuka kwenda kwa wananchi kuwasikiliza changamoto zao na kuzitafutia majawabu.
Chongolo amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha wanawahudumia wananchi na kutatua changamoto zao ili kuendelea kutekeleza nia na dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuwatumikia Watanzania na kuyafikia malengo yanayokusudiwa.
Chongolo amesema katika maeneo waliotembelea kuna miradi ambayo imekamilika lakini kuna maeneo ambayo miradi haijakamilika hivyo wametoa maelekezo kwa viongozi husika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa haraka, kadri ilivyopangwa.
Amesema miradi hiyo ni pamoja na ile inayohusu huduma ya maji ambapo wametoa maelekezo mahsusi kuhakikisha inakamilika na wananchi wanapata maji.
Kwenye eneo la elimu amesema kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika, ambapo mabilioni yaliyoshushwa kwa kipindi hiki kifupi shule zimejengwa kwenye kila kata na watoto wanaendelea kupata elimu bila malipo.
Kwa upande wa nishati ya umeme mkoani Rukwa, Ndugu Chongolo amesema hapo kabla ulikuwa na changamoto lakini kwa sasa imepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na serikali kuwekeza kwenye mpango wa kusambaza umeme vijijini, ambapo vijiji vilivyobaki ni chini ya 30 hivyo ameelekeza mpaka kufika Disemba 30 vijiji vyote 339 mkoani humo, vipate umeme.
Amesema maelekezo ya Rais ni kuhakikisha umeme unamfikia kila mwananchi, ndiyo maana Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuongezwa Kwan hizo za umeme kutoka 20 kila kijiji hadi 60 ili kuongeza wigo wa upatikanaji wake kwa kila kijiji kilichofikiwa, hatimae Keri ya ukosefu wa nishati hiyo, Uwe historia.
“Kazi mnafanya, kikubwa ni wajibu wa serikali kuleta miradi ili mneemeke na shughuli mnazofanya, kuna suala la mahindi wapo watu wawajalipwa tunaiagiza wizara ya kilimo kuwalipa haraka ili watu waendelee na msimu ujao wa kilimo.”
“Tunaiagiza tena Wizara ya kilimo wahakikishe mahindi yailiyoko kwa wananchi yananunuliwa na mbolea mwaka huu waisogeze kwa wananchi sio iishie wilayani.”
Aidha Chongolo ametoa kwa Naibu Waziri TAMISEMI kuhakikisha wanajenga vituo vya afya Senga na Sumbawanga Asili ili kutatua changamoto ya wananchi kukosa vituo vya afya katika maeneo hayo.
Aidha amewataka Viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika mkoa huo wajenge mazingira ya wananchi kuwafikia na kueleza changamoto zao.