Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wafanyakazi wake 11 wameuawa katika shambulio la mabomu la utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza.
Umoja wa Mataifa ulitangaza jana Jumatano kwamba wafanyakazi tisa wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza.
UNRWA imesema kuwa Ukanda wa Gaza utashuhudia janga la binadamu iwapo hazitafunguliwa njia ya amani kwa ajili ya kupeleka misaada kwa Wapalestina wa eneo hilo.
Msemaji wa UNRWA, Adnan Abu Hasna amesema: Ukanda wa Gaza utashuhudia janga la binadamu ambalo halijawahi kuonekana ikiwa njia salama hazitafunguliwa kwa ajili ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu, chakula na maji.
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia limetangaza kuwa, wafanyakazi wake kadhaa wa misaada ya kibinadamu huko Gaza wameuawa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza ilitangaza jana kwamba, idadi ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo hilo imefikia 1,555.
Wizara hiyo imesema katika taarifa yake kuwa: Watu elfu 5,184 wamejeruhiwa tangu kuanza hujum ya kinyama ya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.