Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa kukatwa umeme katika eneo hilo, lililowekewa mzingiro na marufuku ya kila kitu na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel, kutasababisha vifaa vya mahospitali vishindwe kufanya kazi na kuhatarisha maisha ya wagonjwa wa Kipalestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la SAMA, Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imesema: kukatwa umeme katika ukanda huo na utawala haramu wa Kizayuni kutasababisha mashine za kuua viini vya maradhi na vituo vya usambazaji oksijeni na maji katika hospitali vishindwe kufanya kazi.
Wizara hiyo imebainisha kuwa: kukatwa umeme kutapelekea kusimamishwa pia huduma za kusafisha damu na kupoteza maisha wagonjwa wa figo 1,100, ikiwa ni pamoja na watoto 38 wanaohitaji usafishaji mara tatu kwa wiki.
Maisha ya watoto 100 wanaozaliwa kabla ya wakati katika wodi za watoto nayo pia yako hatarini kutokana na kukatika umeme katika vituo vya afya.
Taasisi hiyo ya tiba ya Palestina imeongezea kwa kusema: “kukatwa umeme kutasimamisha huduma za maabara 58 na benki za damu. Wakati huohuo, maelfu ya watu waliojeruhiwa na wagonjwa wanahitajia sana kufanyiwa vipimo vya kitiba na kutiwa damu mwilini, kwa hiyo kukatika umeme kutasimamisha huduma za uchunguzi zinazofanywa na timu ya matabibu kuhusiana na majeraha waliyopata majeruhi hao.”