Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa serikali inalipa kwa wakati madai yote yanayowasilishwa na Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi) lenye urefu wa kilomita 3.0 na Barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 1.66 lililopo jijini Mwanza ambapo ujenzi umefikia asilimia 78 ya Utekelezaji
Ameyasema hayo Oktoba 11, 2023 akiwa Mwanza katika ziara ya kukagua Daraja hilo linalounganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita katika Ziwa Victoria kwa kugharimiwa na Serikali kwa jumla ya shilingi Bilioni 716.3
Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Ujenzi wa Daraja hilo ameupa kipaumbele kikubwa kwa kuhakikisha Mkandarasi hatoki nje ya mradi kwa kutoa fedha kuwezesha madai yote ya mkandarasi kulipwa ndani ya muda ili kuhakikisha anafanya kazi bila kusimama.
“Mheshimiwa Rais anaendelea kuonesha kwa vitendo kaulimbiu yake ya awamu ya sita ya kazi iendelee ambayo inamaanisha kijiti ambacho alikipokea kutoka kwa kaka yake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ameendeleza pale alipoishia ikiwemo mradi huu wa historia kwa nchi yetu” Amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais anahakikisha hakuna madai yanayowasilishwa na mkandarasi huyo ambayo hayalipwi na amemuomba Mkuu wa Mkua wa Mwanza, Amos Makalla, kupita mara kwa mara katika mradi huo ili kuhakikisha kazi inaendelea kwa sababu mkandarasi hana sababu yeyote ya kutoendelea na kazi kwani malipo yote yanafanyika kwa wakati.
Amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuifungua Mikoa ya kanda ya ziwa ambapo kwa muunganiko wa Bandari pamoja na mradi wa Reli ya kisasa ya SGR, mizigo kutoka nchi mbali mbali duniani itatumia miundombinu hiyo kusafirisha mizigo yao na hivyo kunufaisha ukanda huu wa ziwa kwa kupitia kituo kikubwa cha SGR cha Misungwi.
Awali akitoa taarifa ya daraja hilo, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Eng Boniface Mkumbo amesema kuwa hadi sasa mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi bilioni 396.3 ambazo zinajumuisha malipo ya awali pamoja na hati zote za madai 17 alizowasilisha.