Utawala wa Kizayuni wa Israel umeuambia Umoja wa Mataifa kuwa, kuna haja kwa wakazi wote wa eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kuondoka na kwenda katika maeneo mengine ya ukanda huo katika kipindi cha saa 24 zijazo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema katika taarifa kuwa, “Jeshi la Israel limeitaarifu UN kuwa, wakazi wote milioni 1.1 wa Wadi Gaza, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza wahamie kusini mwa Gaza, ndani ya saa 24 zijazo.”
Dujarric ameongeza kuwa: Umoja wa Mataifa unaamini kuwa, ni muhali kwa hatua kama hiyo (ya idadi kubwa ya watu kuhama) kufanyika pasi na kushuhudiwa janga la kutisha la kibinadamu.
Mashambulizi ya kikatili ya utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wasio na ulinzi wa eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu yangali yanaendelea.
Wapalestina zaidi ya 1,570 wameuawa shahidi mpaka sasa, mbali na wengine zaidi ya 6,600 kujeruhiwa, huku utawala katili wa Israel ukiendelea kuwashambulia kwa mabomu na makombora Wapalestina wa Gaza.
Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, utawala haramu wa Israel ulitangaza kuliwekea mzingiro kamili eneo la Ukanda wa Gaza kwa kusitisha ufikishaji wa chakula na maji na pamoja na huduma ya umeme, na kuzua hofu ya kuwa mbaya zaidi hali ya kusikitisha na kukatisha tamaa ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika eneo hilo.
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk akizungumzia mzingiro huo hivi karibuni alisema, mzingiro wa kila kitu ambao Israel imeamua kuuwekea Ukanda wa Gaza, na kuwanyima raia bidhaa muhimu kwa ajili ya maisha, umepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa.