Maafisa wa upelelezi kutoka kwenye Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya wameanzisha msako wa mwanafunzi wa chuo kikuu ambae amekuwa akifanya kazi kama wakili bila leseni huku akitumia stakabadhi za wakili kinyume cha sheria.
Hali ya taharuki imeibuka katika Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) baada ya mwanaume huyo anayedaiwa kuwa wakili ‘kishoka’ anaetamba nchini Kenya.
Usiku wa kuamkia leo LSK tawi la Nairobi lilitoa taarifa kupitia mtandao wa X, likitahadharisha umma kuhusu mtu huyo anayedaiwa kujifanya Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya ili kuwatapeli wateja wasio na hatia. Taarifa hiyo iIlieleza kuwa mwanaume anayejulikana kwa jina Brian Mwenda Njagi hakuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, wala sio mwanachama wa jamii.
Habari hii iliingia kwenye headlines baada ya makumi ya watu kuanza kushiriki kazi za zamani za wakili huyo anayedaiwa kuwa feki, huku video zikimuonyesha sio tu akiwa mahakamani akimwakilisha mteja bali pia katika matukio kadhaa ambapo anaweza kuonekana akichangia hoja kwenye mikutano ya LSK. na pia kugombana na afisa wa polisi baada ya ugomvi, Mkanda mzima wa kesi ya Brian Mwenda inawakumbusha wadau wengi series maarufu kutokea nchini Marekani ‘Suits’ ambapo kijana Mike Ross alikuwa ‘wakili mahiri na hodari’ aliyekuwa akiwawakilisha wateja wake mahakamani ingawa hakuwa na vyeti wala leseni.
Katika video moja ambayo imewaacha wengi kwenye mshangao, kijana huyo alinaswa kwenye televisheni moja kwa moja akimwakilisha mteja mashuhuri, kiongozi wa zamani wa Mungiki Maina Njenga.
LSK Nairobi pia lilihimiza yeyote ambae alikuwa na taarifa kuhusu Njagi au mtu mwingine yeyote anayejifanya wakili kuripoti kwa mamlaka husika ili kuchukuliwa hatua.