Mapigano makali bado yanaendelea nchini Sudan, ikiwa ni miezi sita sasa na bila kuonyesha dalili zozote za suluhisho la amani, na kuwa moja ya migogoro mibaya zaidi nchini humo.
Mapigano hayo yaliyoanza April 15 mwaka huu kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na maeneo mengine, yamesababisha vifo vya maelfu ya raia, mamilioni wengine kukosa makazi, na kuharibu miundombinu muhimu nchini humo, hususan mjini Khartoum.
Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan imesema kupitia mtandao wa X kuwa, karibu watu milioni 5.6 wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan tangu mapigano hayo yalipoanza, na kwamba mashirika ya kibinadamu yameweza kuwafikia watu milioni 3.6 na kuwapa msaada wa kuokoa maisha.