Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua ‘mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada’ na kusema katika mwaka wa masomo 2023-2024 jumla ya TZS 48 bilioni zmetengwa kuwanufaisha wanafunzi 8,000 wa ngazi ya stashahada.
Mwongozo huo unapatikana katika tovuti za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (www.heslb.go.tz) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) – www.nactvet.go.tz.
Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Mwongozo huo zilizofanyika jijini Dar es salaam, Prof. Mkenda amesema wanafunzi watakaonufaika na mikopo hiyo ni wale wanaosoma fani za Afya na Sayansi Shirikishi (Health and Allied Sciences); Elimu (Education); Usafiri na Usafirishaji (Transport & Logistics); Uhandisi na Nishati (Energy Engineering); Madini na Sayansi ya Ardhi (Mining & Earth Science); na Kilimo na Mifugo (Agriculture & Livestock).
“Katika fani hizi, kuna programu mahsusi ambazo zipo kwenye Mwongozo ambazo tungependa wanafunzi wasizome … hivyo ni muhimu kuusoma Mwongozo ulipo kwenye tovuti ili kuzifahamu…” amesema Prof. Mkenda katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Prof. Mkenda ameongeza: “Serikali imejenga Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya nchini kote ambavyo vinahitaji wataalamu. Serikali pia imejenga na kukarabati Shule ambazo zinahitaji walimu wa Sayansi. Serikali pia inatekeleza mageuzi makubwa katika Sekta za Mafuta, Gesi na Madini na sekta ya Kilimo kupitia mpango wa BBT – Building Better Tomorrow… hivyo tunahitaji wataalamu katika maeneo haya,”.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB ambayo ndiyo itatoa mikopo hiyo, Prof. Hamisi Dihenga HESLB ipo tayari kutekeleza uamuzi huo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao kuanzia Oktoba 7 – 22, 2023 na kuwa HESLB itaanza kutoa elimu kuhusu uombaji sahihi wa mikopo hiyo.