Umoja wa Mataifa umesema mzozo kati ya Israel na Hamas umefikia hatua mbaya wakati Hospitali za Gaza zikikaribia kuishiwa akiba ya nishati na juhudi za kupitisha misaada ya kiutu katika mpaka wa Rafah zikiendelea.
Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu Antonio Guterres umetoa wito kwa kundi la Hamas liwaachilie huru Mateka huku ukiitaka Israel kuruhusu misaada ifike katika Ukanda wa Gaza.
Guterres amesema Umoja huo una chakula, maji, dawa na mafuta ambayo tayari yako Misri na katika ukingo wa magharibi kwa ajili ya kupelekwa Gaza kama Wafanyakazi wake wataruhusiwa kuvisafirisha bila ya vikwazo.
Guterres ametoa kauli hiyo wakati ambapo zaidi ya Watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao huku Israel ikitarajiwa kufanya uvamizi unaolenga kuliangamiza kundi la Hamas, lililovamia kusini mwa Israel zaidi ya wiki moja iliyopita.
Wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umetolewa wakati Mashirika ya misaada ya kiutu yakifanya juhudi za kuingiza misaada Gaza katika mzozo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 2,600, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imevinukuu vyombo vya habari vya Misri vilivyoripoti kuwa huenda mpaka wa Rafah kuingia Gaza ukafunguliwa kwa muda leo Jumatatu.