Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifungua nchi kwa mtandao wa barabara ambapo amezindua daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 na barabara za maingilio zenye urefu wa Kilomita moja kwa kiwango cha lami lililojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 11.14, leo Oktoba 16, 2023
Kukamilika kwa daraja hilo lililopo Barabara ya Mkoa ya Kitukutu – Gumanga – Nyahala (Sibiti) inayounganisha Mkoa wa Singida, Mwanza na Mara kupitia Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82 na kilomita 25 kuunga daraja ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha na kuunganisha Barabara Kuu na za mikoa Nchi nzima.
Rais Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Singida kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuona faida ya daraja hilo lililopo kijiji cha Msingi wilaya ya Mkalama.
Barabara hiyo ni barabara muhimu kwani inaanzia kwenye Barabara kuu ya Singida kwenda Nzega na inaunganisha Barabara itakayojengwa kwa utaratibu wa EPC+F inayoanzia Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti – Lagalo – Maswa yenye urefu wa Kilometa 389 ambazo ni barabara muhimu kiuchumi na kijamii.
Awali akitoa taarifa ya Mradi huo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuweka taa katika madaraja hayo yanatekelezwa na tayari daraja la Msingi limewekwa taa na madaraja mengine yatawekwa taa mara baada ya Mkandarasi kukamilisha ujenzi.
Bashungwa amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi hiyo pamoja na miradi mingine aliyoelekeza itekelezwe kwani inazidi kuunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa, mikoa ya Kati na kanda ya Kaskazini na kusema kuwa Rais ni mtu wa kazi na anatekeleza ahadi zake kwa vitendo.