Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa nchini Israel siku ya Jumatano kwa ziara ya mshikamano baada ya shambulio baya la Hamas mnamo Oktoba 7, kabla ya kusafiri hadi Jordan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ametangaza.
“Rais atathibitisha tena mshikamano wa Marekani na Israel na ahadi yetu isiyotetereka kwa usalama wake,” Antony Blinken amesema mapema Jumanne, baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv Jumatatu usiku.
“Israel ina haki na wajibu wa kuwalinda raia wake dhidi ya Hamas na magaidi wengine na kuzuia mashambulizi ya siku zijazo,” ameongeza mkuu wa diplomasia ya Marekani.
Joe Biden “atasikia kutoka kwa Israeli kile inachohitaji kutetea raia wake na tutaendelea kufanya kazi na Baraza la Congress ili kukidhi mahitaji hayo,” ameongeza.
Ametangaza kuwa Marekani pia imepata dhamana kutoka kwa Israel kuhusu kufikisha misaada ya kibinadamu ya kigeni katika Ukanda wa Gaza iliozingirwa, wakati ambapo Israel inatayarisha mashambulizi ya ardhini dhidi ya eneo linalotawaliwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas.
Joe Biden anatarajia “kusikia kutoka kwa Israel jinsi itakavyoendesha operesheni zake kwa njia ambayo itapunguza majeruhi ya raia na kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia huko Gaza kwa njia ambayo hainufaishi Hamas,” amesema Antony Blinken.