Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa serikali ya Ethiopia na wenzi wake kudumisha juhudi za uratibu wa pamoja ili kudhibiti mlipuko unaoendelea wa kipindupindu nchini humo.
Katika taarifa yake kuhusu milipuko ya magonjwa na majanga mengine katika bara la Afrika iliyotolewa jumapili, WHO imesema Ethiopia inashuhudia moja ya milipuko ya kipindupindu uliodumu kwa muda mrefu katika historia, ambapo kesi ya kwanza iliripotiwa mwezi Agosti mwaka jana.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika hilo, kuanzia mwezi Agosti mpaka mwisho wa mwezi Desemba mwaka jana, jumla ya kesi 1,073 za kipindupindu ziliripotiwa na watu 30 wamefariki kutokana na ugonjwa huo, huku kesi zilizoripotiwa mpaka kufikia Septemba 21 mwaka huu zikifikia 23,652 na watu 299 wamefariki kutokana na kipindupindu.