Marekani na Israel “zimekubali kuandaa mpango utakaowezesha misaada ya kibinadamu kutoka kwa mataifa wafadhili na mashirika ya kimataifa kuwafikia raia wa Gaza,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitangaza katika ziara yake nchini Israel Jumanne.
Hata hivyo, haijulikani kama kuna maendeleo yoyote yalifanywa kwenye ufunguzi wa kivuko cha Rafah – njia pekee inayoweza kutumika ya kuingia Gaza.
Blinken alisema makubaliano ya kufanyia kazi mpango huo yalifanywa kwa ombi la Marekani, na “wanakaribisha kujitolea kwa serikali ya Israel kufanyia kazi mpango huu.”
“Ni muhimu kwamba misaada ianze kuingia Gaza haraka iwezekanavyo,” Blinken alisema, akibainisha kuwa Marekani inashiriki “wasiwasi wa Israel kwamba Hamas inaweza kunyakua au kuharibu misaada inayoingia Gaza au kuzuia isiwafikie watu wanaoihitaji.”
“Ikiwa Hamas kwa njia yoyote ile itazuia usaidizi wa kibinadamu kuwafikia raia, ikiwa ni pamoja na kunyakua misaada yenyewe, tutakuwa wa kwanza kulaani. Na tutajitahidi kuzuia hilo lisitokee tena,” alisema.
Rais wa Marekani Joe Biden “anatarajia sana kulijadili zaidi” wakati wa ziara yake nchini Israel, Blinken alisema.