Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza namna Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyofanikiwa kutekeleza miradi ya ujenzi ya barabara mkoani Singida katika kipindi kifupi.
Akizungumza katika madhimisho ya miaka 60 ya Mkoa wa Singida, Waziri Bashungwa alisema wananchi wa mkoa huo wanakila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa namna alivyotekeleza miradi ya ujenzi mkoani humo.
Akifafanua baadhi ya miradi hiyo, Waziri Bashungwa alisema Rais Samia wakati anaweka jiwe la msingi kujengwa kwa kiwango cha lami Barabara ya Mkiwa-Itigi-Rungwa ikiwa ni sehemu ya Barabara ya Mkoa wa Singida pamoja na Mbeya kuanzia Mkiwa-Itigi hadi Makongorosi.
Alisema wakati wa hafla hiyo Rais Samia alimpa maelekezo (yeye) pamoja na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo aendelee mpaka Makongorosi ili kuunganisha Mkoa wa Singida pamoja na Mbeya.
Kadhalika, Waziri Bashungwa maelekezo hayo ya Rais Samia pia yatawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Tabora kwa sababu itaunganisha Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati pamoja Kanda ya Nyanda za juu kusini.
“Hii ni zawadi kubwa sana kwa wana Singida wanaposherekea miaka 60 ya kuanzishwa kwa mkoa pokeeni zawadi ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Waziri Bashungwa.
Aliongeza kuwa Rais Samia wakati anazindua Daraja la Msingi (mita 100) linalounganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu alielekeza kuwa katika vipaumbele vya kuunganisha mikoa hiyo Wizara ya Ujenzi iongeze nguvu na kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Iguguno-Nduguti- Umanga-Mkalama- Sibiti kuunganisha mikoa hiyo.
Alisema Rais Samia zawadi nyingine aliyowapatia wananchi wa Singida ni kuanza ujenzi wa kilometa 10 kwenye makao ya Wilaya Nduguti na kuelekeza kuletewa nyaraka Ili atoe kibali na kilometa hizo zianze kujengwa wakati zinatafutwa fedha ya kuendelea na kilometa 76 zilizobaki katika kipande hicho cha barabara.
Kadhalika, Waziri Bashungwa alitaja zawadi nyingine ni barabara inayounganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa kupitia Singida kuelekea Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Arusha kuanzia Karatu-Mbulu-Hydom – na kipande cha kilometa 78 kinachopita Mkoa wa Singida mpaka Daraja la Sibiti kupitia Meatu-Ng’hoboko-Simiyu hadi Wilaya ya Maswa