Kampuni ya ALAF Limited, ambayo ni sehemu ya makampuni ya Safal Group na mtoa huduma bora wa huduma za ujenzi nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, imezindua mradi wa mabati ya rangi wenye thamani ya mabilioni ya shilingi unaolenga kuokoa Zaidi ya dola milioni 190 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi huo mkubwa ilihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mh. Dk Doto Biteko pamoja na uongozi wa juu wa kampuni ya ALAF Limited, wateja na wadau mbalimbali.
Akiongea katika hafla hiyo, Naibu Waziri Mkuu Biteko aliipongeza Kampuni ya ALAF Limited kwa kuwekeza katika mradi huo, Naibu Waziri Mkuu alisema uwepo wa uwekezaji mkubwa kama huu ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh Dtk. Samia Suluhu Hassan, katika kufungua milango, kuweka mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji kufanya biashara kwa uhuru zaidi.
“Uwekezaji wa nanmna hii ni wa kupigiwa chapuo kwakua unawekezwa Tanzania kwa manufaa ya watanzania,” alisema.
Alisema uwekezaji wa dola za Kimarekani milioni 25 unaonesha ni kwa namna gani sekta ya viwanda hasa uzalishaji na uongezaji wa thamani unavyokuwa kwa kasi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited Ashish Mistry alisema mradi huo unaokadiriwa kugharimu dola milioni 25 na ambao uzalishaji wake kibiashara unatarajiwa kuanza Desemba 2024, unalenga kuimarisha miundombinu ya kiwanda kilichoko sasa ili kiwe na mwonekano wa kisasa.
“Lengo kuu la mradi huu ni ujumuishaji mradi wa kuweka nakshi bidhaa za chuma zinazozalishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya mpango kabambe wa kampuni yetu”, alisema na kuongeza, mradi pia umelenga kutoa huduma za kuweka nakshi ya rangi kwa bidhaa za chuma zikiwemo zile zinazotumika kwenye vyombo vya majini kwa kuzingatia changamoto za kimazingira yaliyoko maeneo ya pwani ya Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alibainisha zaidi kuwa moja wapo ya vipengele muhimu katika mradi huo wa mabati ya rangi ni kuhakikisha hauathiri mazingira na ili kufikia azma hiyo, uongozi utatumia malighafi ambazo hazitaathiri mazingira kwa namna yoyote ile.