Lionel Messi ameondoa uvumi kwamba ataondoka Inter Miami kwa mkopo kwenda kuchezea klabu nyingine mara tu msimu wa MLS utakapomalizika.
Inter Miami, ambao hawakufika hatua ya mtoano ya MLS, watamenyana na Charlotte FC katika mchezo wao wa mwisho Jumamosi.
Huku Messi akitarajiwa kuichezea Argentina katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi Novemba, kulikuwa na uvumi kwamba nyota huyo wa zamani wa Barcelona anaweza kurejea Ulaya kwa mkopo wakati wa mapumziko ya msimu wa MLS ili kuendelea kuwa fiti kwenye mechi.
Hata hivyo, alipoulizwa kama anafikiria kuchezea klabu nyingine wakati wa Desemba [kati ya msimu wa MLS wa 2023 na 2024] baada ya Inter Miami kushindwa kufuzu kwa mechi za play off, Messi alisema: “Hapana.
“Ni aibu [hatukufuzu]. Tulikaribia sana. Nilikosa michezo michache iliyopita, tulikuwa na majeraha kadhaa.
Mwezi wa Julai ulikuwa mgumu sana kwetu, tulicheza kila siku tatu, tulisafiri. Lakini ilishinda mchuano ambao ni muhimu kwa klabu na kwa kile kitakachokuja mwaka ujao,” alisema baada ya ushindi wa 2-0 wa Argentina dhidi ya Peru katika kufuzu kwa Kombe la Dunia Jumanne.
“Nitafanya mazoezi, nitacheza mechi yetu ijayo [dhidi ya Charlotte FC] na nitajaribu kufika hapa timu ya taifa kwa njia bora zaidi kwa mwezi wa Novemba.
Baada ya hapo, nitafurahia likizo nchini Argentina kwa mara ya kwanza ambapo nitakuwa na siku nyingi za mapumziko mwezi wa Disemba, nikiwa na likizo, nikiwa na amani ya akili, na watu wangu.Mwezi Januari, nitarudi tena kufanya preseason. “