Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani siku ya Jumatano lilitoa wito wa dola milioni 19 kutoa msaada wa dharura kwa makumi ya maelfu ya watu walioathiriwa na mfululizo wa matetemeko makubwa ya ardhi na mitetemeko ya ardhi ambayo imetikisa magharibi mwa Afghanistan.
Ana Maria Salhuana, naibu mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani nchini Afghanistan, alisema lilikuwa linasaidia waathirika lakini linahitaji ufadhili zaidi kwa sababu “tunalazimika kuchukua chakula hiki kutoka kwa mpango ambao tayari haufadhiliwi sana.”
Kikundi hicho kilisema kinafanya kazi ya kutoa msaada wa dharura wa chakula kwa watu 100,000 katika mkoa huo.
“Majanga kama haya matetemeko ya ardhi yanazikumba jamii ambazo tayari hazina uwezo wa kujilisha katika ufukara mkubwa,” WFP ilisema.
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 katika kipimo cha Richter lilipiga sehemu ya magharibi mwa Afghanistan siku ya Jumapili, baada ya maelfu ya watu kufariki na vijiji vizima kuathiriwa na matetemeko makubwa wiki moja kabla.
Lilikuwa ni tetemeko la nne ambalo Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani limepima katika kipimo cha 6.3 katika eneo hilo hilo kwa zaidi ya wiki moja.