Uganda inasema juhudi zilikuwa zinaendelea siku ya Jumatano kuhakikisha kwamba wahusika wa shambulizi lililoua watatu katika mbuga ya wanyama siku ya Jumanne “wanawindwa na kuuawa”.
Msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye alisema Jumatano kwamba kikosi cha pamoja cha jeshi, polisi na mamlaka ya wanyamapori “kimepeleka rasilimali zote, kiufundi na kimaumbile, kuwasaka magaidi hao na watahakikisha wanahusika na vitendo vyao viovu”.
Shambulio hilo linalodaiwa kutekelezwa na Allied Democratic Forces (ADF) liliua wanandoa katika fungate yao, ambao walikuwa raia wa Afrika Kusini na Uingereza, pamoja na mwongoza safari wa Uganda katika Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth kusini-magharibi mwa Uganda.
Kundi la waasi la ADF limekuwa na uhusiano na Islamic State (IS) tangu 2019 na lina makao yake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Siku ya Jumatano, IS ilitoa taarifa ikidai kuhusika na mauaji hayo.