Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah siku ya Jumatano alitoa wito wa kukomeshwa kwa kile alichokitaja kama “mauaji” huko Gaza, akisema msaada wa kibinadamu lazima uruhusiwe mara moja katika eneo la Palestina lililozingirwa.
Salah alitoa ujumbe wa video kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, akitoa maoni yake ya kwanza kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas baada ya kukosolewa vikali nchini kwao Misri kwa kukaa kimya kuhusu suala hilo kwa zaidi ya wiki moja.
Wizara ya afya ya Gaza imesema takriban Wapalestina 3,478 wameuawa na 12,065 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, siku ambayo kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas lilipovamia miji ya Israel, na kuua watu 1,400 na kuchukua mamia ya mateka.
Siku ya Jumanne, malori ya Misri yaliyokuwa yamebeba misaada kuelekea Gaza yalisogea karibu na kivuko cha mpaka cha Rafah lakini haikufahamika ni lini au iwapo yataweza kuvuka hadi kwenye eneo hilo, huku Misri ikitaka kupata hakikisho la usalama kutoka Israel baada ya eneo la mpakani kushambuliwa mara nne.
Serikali ya Israel ilisema siku ya Jumatano kwamba Israel haitaacha msaada wa kuingia Gaza kutoka Misri, lakini vifaa hivyo havitaruhusiwa kufika Hamas.
“Sio rahisi kila wakati kuzungumza kwa wakati kama huu, kumekuwa na vurugu nyingi na ukatili mwingi wa kuvunja moyo … Maisha yote ni matakatifu na lazima yalindwe,” Salah alisema.
“Mauaji yanapaswa kukomeshwa; familia zinasambaratika. Kilicho wazi sasa ni kwamba msaada wa kibinadamu kwa Gaza lazima uruhusiwe mara moja. Watu wa huko wako katika hali mbaya sana.”